KUANZA BIASHARA YA VIPODOZI KWA MTAJI MDOGO
Njia Ya Kwanza Ya Kuanza Biashara Ya Vipodozi Kwa Mtaji Mdogo
Hello! Mambo vipi? Vipi shughuli zako zinaendeleaje?
Biashara ya vipodozi ni moja kati ya biashara nzuri hapa nchini kwetu kwa sababu ina wateja wa kutosha, bidhaa zake zinapatikana kwa urahisi na faida yake ni nzuri. Unaweza kununua body spray kwa Tsh 3500 na ukaiuza kwa Tsh 5000 hivyo kupata faida ya Tsh 1500 sawa na 42.8%; yaani ukiwekeza Tsh 700,000 kununua spray 200 utaziuza na kupata Tsh 1,000,000 na faida ya Tsh 300,000.
Vipi, sio nzuri? Ni nzuri!
Ishu kubwa iliyopo ni kwamba vipodozi vipo vingi sana na mahitaji ya wateja wake yanatofautiana sana. Faida kubwa unaweza kuipata kutokana na mauzo ya vipodozi vingi vingi hivyo kukutaka wewe kuwa na vitu vingi dukani mwako ili kunasa wateja mbalimbali. Hapo ndipo mtaji mkubwa unapotakiwa - unaweza kutumia Tsh 8,000,000 na bado baadhi ya vitu usiwe navyo.
Njia Ya Kwanza Ya Kuanza Biashara Ya Vipodozi Kwa Mtaji Mdogo
Unaweza kuanza biashara ya vipodozi kwa mtaji mdogo kama Tsh 3,000,000 kwa kuanza na vipodozi vya jamii moja kwanza. Kwa mfano unaweza kuanza na bidhaa za NIVEA tu - Losheni, Body Spray, Facial Cleanser nk; au kuanza na lotion tu ambazo kwa sasa zinafanya vizuri sokoni - Rinju, Rubee, Nivea, Queen Elizabeth, Razaq nk; au kuanza na body spray tu na kuwa mahiri katika eneo hilo.
Anza na kitu kimoja, fanya vizuri sana na kuwa mahiri katika kitu hicho. Mtaji wako utakutosha kuanzia, kutengeneza faida, kukuza mtaji na hatimaye kuongeza bidhaa zingine taratiiiibu hadi uwe na duka unalolipenda.
Nina imani umewahi kuona maduka ambayo yanauza pafyumu tu na bado yana wateja wengi; hicho ndicho ninachokuambia sasa.
Enhee, Baada Ya Hapo?
Baada ya hapo sasa utakuza mtaji wako, idadi ya wateja wako, maarifa yako ya biashara ya vipodozi na kadhalika. Amini nakuambia, utakuja kuona urahisi mkubwa sana baadae.
Biashara ya vipodozi inabadilikabadilika sana na unatakiwa kusoma wateja wako, wateja wapya na mwenendo mzima wa soko. Queen Elizabeth Lotion unayoiona leo inatamba jua kwamba mwaka 2005 haikuwa hivyo sokoni; losheni ya E9 ambayo leo huioni ikitamba sana jua kwamba miaka ya 2000-2005 ilitamba vizuri tu. Kwa hiyo na wewe jiandae kubadilika kulingana na mazingira ya biashara.
Biashara ni mahitaji, bidhaa/huduma na mauzo/faida; Tumia Tsh 3,000,000 yako kununua na kuuza vipodozi ambavyo vitakidhi mahitaji ya watu wako na kukuzalishia faida.
Ukihitaji msaada wa kupangilia vizuri mwanzo wako utaupata. Na ukianza vizuri nafasi yako ya kufanikiwa inakuwa nzuri zaidi. Kila la kheri!
Hellow umetoa funzo zuri Sana Ila ungeacha mawasiliano ama email address ingekuwa poa zaidi
Asante sana kwa ushauri mzuri wa biashara hii ya vipodozi! At least kuna kitu nimejifunza; mimi ndiyo kwanza nimeanza biashara hii.