Hauna wateja wengi kwa sababu mbalimbali kama vile kukaa tofauti na walipo wateja wako, kutokujulikana, wateja wako kuwa wanapata mahitaji yao sehemu zingine, kutokuwa na sababu maalum za wateja kuendelea kupendelea bidhaa/huduma zako na kadhalika.
Sasa ukitaka kutatua hayo mambo na kuongeza wateja basi wekeza katika:
1. Uzuri wa bidhaa/huduma zako (Upatikanaji, Ubora na Gharama)
2. Kufikia wateja wengi zaidi
3. Kuvutia wateja waje kwako
Hii dunia haijawahi kuwa na uhaba wa wateja. Ni wewe tu na hospitali yako au duka lako hamjawahi kuwafikia na kuwapa kila sababu ya kuja kwako. Kama hakuna anayekujua basi sahau kuhusu wateja. Kama ubora wa huduma zako ni mdogo basi wateja wako wataondoka. Kama bei zako haziendani na bei zilizopo vichwani mwa wateja wako basi wataondoka tu.
Hospitali nyingi za watu binafsi (private hospitals) zinapendwa zaidi na wateja kwa sababu ya uharaka wa kupata huduma, ubora wa huduma, mazingira mazuri, majibu mazuri kutoka kwa wauguzi na kadhalika. Na kwa sasa kinachoongeza zaidi wateja ni kuhudumia wagonjwa wa bima za afya – NHIF, Britam, Jubilee, Smart, Strategis nk. Pia kuwahi kuanza kutoa huduma na kutoa huduma kwa muda mrefu. Kila ukienda daktari unampata, mapokezi unaandikishwa chap chap na unaingia chumba cha daktari anakuhudumia chap chap.
Ukiwa na huduma nzuri wateja watakuja tu. Na watawaambia wenzao pia wawe wanakuja hapo. Yaani unatangaziwa biashara yako bure kabisa!
Kama haujulikani na/au umeweka biashara yako katika eneo ambalo halina idadi kubwa ya wakazi wala wanaofanya shughuli zao hapo au kupita njia basi utakuwa na changamoto kidogo kupata wateja. Watatoka wapi sasa? Ndio maana tunasema unapotaka kuanzisha biashara yako basi location ni muhimu sana. Weka biashara yako mahali ambapo wateja wako wanakaa au wanapita. Ikitokea tayari umeshakosea kwenye hilo au una plan nyingine basi hakuna shida, buni namna ya kufikia wateja wengi zaidi kupitia kujitangaza na kuvuma. Gawa vipeperushi, post katika mitandao ya kijamii, shiriki katika matukio ya kijamii, tumia watu maarufu au watu wenye watu wengi na ushawishi wasemee biashara yako, shiriki katika mikutano ya biashara, shiriki katika mikutano ya mabaraza ya wataalam, fanya ushirika na biashara zenye wateja wengi tayari wanaofanana na wateja wako na kadhalika. Jibrand vizuri na nenda maeneo ambao wateja wako wapo kawaambie kuhusu biashara yako. Watakuja. Wakija wape huduma nzuri sana ili warudi tena na tena na wawatangazie wenzao.
Wekeza katika uzuri wa bidhaa/huduma zako na matangazo. Unaweza kufanya biashara ukiwa popote pale. Kama una wasi wasi au unahitaji msaada zaidi basi cheki nasi tutakusaidia hiyo kazi ya kuboresha huduma zako na kukutangaza.
Kuna kitu kimoja tofauti. Umewahi kuona watu wanapita biashara yako na kwenda kupata bidhaa/huduma kama zako sehemu nyingine tofauti na yako? Yaani tayari wanakujua ila wanakupita. Inaumiza sana moyo. Ila ndo hivyo, mteja anaenda ambapo ana maslahi napo. Si ajabu issue sio bidhaa au huduma zako, bali ni mahusiano pamoja na urahisi wa kupata vitu vingine huko. Yaani kama unavyoona watu wakiacha maduka ya nguo, viatu, mikoba nk mitaani kwao na kwenda kununua Kariakoo. Tena sio anaenda kununua kwa jumla, hapana; anaenda kununua mkoba mmoja tu, kwa reja reja. Bei sawa tu na dukani kwako.
Hapa unahitajika kuvutia wateja hawa waje kwako kwa kuwapa sawa na au zaidi ya kile wanachofuata huko wanakoenda. Inaweza kuwa mvuto wa eneo, uchangamfu, discount, offer, mahusiano mazuri, zawadi, mvuto kwa nje na ndani, kuokoa muda, gharama ndogo na kadhalika. Unachotakiwa kukifanya ni kutafiti kwa nini wanakupita wewe na kwenda mbele, wewe umekosa nini, huko wanapata nini cha ziada, gap liko wapi na kisha ziba hilo gap.
Boresha uzuri wa bidhaa/huduma zako, fikiwa wateja wengi zaidi na vutia wateja waje kwako kisha njoo mezani tufurahie mafanikio ya biashara yako pamoja.
Hiyo ndio namna ya kuongeza wateja katika biashara yako. Je, utaweza kutekeleza sasa na kuangalia matokeo katika biashara yako? Kama unahitaji msaada zaidi basi cheki nasi tutakusaidia hiyo kazi ya kuboresha huduma zako na kukutangaza.
Tunakutakia utekelezaji mwema!