Rafiki yangu alianza biashara ya famasi mwaka 2017. Alianza na duka moja ambalo lilikuwa barabarani kabisa eneo lenye idadi kubwa ya wakazi na pia wapiti njia wengi. Wakati anaanza hakukuwa na famasi nyingine karibu, ni yeye tu. Pia aliingia mkataba na NHIF kwa hiyo akawa anapata na wateja wengi pia wa NHIF ambao walikuwa wanakosa dawa hospitali. Akawa anapata faida nzuri tu na mambo yakawa poa sana.
Mwaka 2020 mambo yakawa poa zaidi kwake akafungua famasi nyingine so jumla zikawa mbili.
Hii pia alipata location nzuri kwenye makazi ya watu wengi na wapiti njia wengi, barabarani kabisa. Ila hakuwa anatoa huduma kwa wateja wa NHIF, hii ilikuwa ni wateja wa cash tu. Mambo yakawa poa famasi zote mbili zikakaa sawa vizuri tu.
Mwaka 2021 akapata eneo zuri zaidi mjini katika business centre moja kodi Tsh 800,000 kwa mwezi na wateja wa NHIF wangeweza kupafikia kwa urahisi zaidi maana ni city centre pale. So akachukua mkopo na kuanzisha famasi yake ya tatu, na kama kawaida akaingia mkataba na NHIF ili kuhudumia wateja wa NHIF. Hili eneo lina wakazi wengi around na wapita njia wengi sana, wa miguu na wa magari. Gharama zake za uendeshaji kwa mwezi ni around TZS 3,100,000 (Kodi ya jengo TZS 800,000 + Kulipa wafanyakazi TZS 2,000,000 + Bills TZS 100,000 + Mengineyo TZS 200,000). Hapo bado kuna riba ya mkopo ambao alikopa kwa ajili ya kuanzishia hii famasi.
Famasi ya tatu ikaanza kwa wastani kwa kutegemea sana wateja wa NHIF maana ile business centre haikuwa na watu wengi wanaokuja mule ndani na wapiti njia wengi walikuwa ni wapiti njia tu hawakuwa wanaingia mule famasi kwenda kununua dawa. So taratiibu baada ya miezi sita mahesabu yakaonesha duka linaendeshwa kwa hasara kidogo (Gharama za uendeshaji ni kubwa kuliko faida) bado biashara haijabreak-even, na pia ina mteja mkubwa mmoja tu anayeipa uhai biashara ile – wateja wa NHIF waliokosa dawa hospitali. Duka bado halikuwa na uwezo wa kulipia gharama zake za uendeshaji. Tumaini la pekee lilikuwa ni kujulikana zaidi kadiri muda unavyoenda na kuongeza idadi ya wateja wa NHIF wanaokuja kuchukua dawa pale. Hadi kufikia mwezi wa nne mwaka huu malipo ya wafanyakazi yakaanza kusuasua na ununuzi wa dawa pia ukawa wa kusuasua. Hadi NHIF walipe ndipo ipatikane pesa ya kulipa mishahara na kununua bidhaa za kuweka dukani.
Tarehe 1 Juni 2022 NHIF wakaacha utaratibu wa wagonjwa wanaokosa dawa hospitali kwenda kuchukua dawa hizo famasi za nje zinazohudumia wateja wa NHIF. Duka la rafiki yangu likapoteza zaidi ya 60% ya mapato yake na hakukuwa na plan B ya haraka haraka. So duka likapoteza kabisa matumaini ya kuinuka na kufanikiwa. Huo ndo ukawa mwisho wake na hatimaye rafiki yangu akalifunga rasmi. Alishalipia kodi ya miezi 6 mingine (1 Machi 2022 – 31 Agosti 2022) ila hakuna jinsi imebidi aachie hata hiyo miezi iliyobaki ili kujinusuru na hasara zaidi.
SASA KARIBU TUJADILI ……
Biashara = Faida = Mauzo – Bei za kununulia bidhaa – Gharama za uendeshaji.
1. Umepata picha gani kuhusu location ya kuweka biashara, gharama za uendeshaji, wateja, mauzo, tathmini ya biashara na kufunga biashara?
2. Unaona nini kimesababisha rafiki yangu kufeli katika biashara yake hii ya tatu?
3. Umepata mafunzo gani katika kuelekea kuanzisha biashara yako?
Nasubiri majibu yako tujadili ……
- AFYA ZAIDI (AZ) CONSULTANTS.