ANGALIA USIUZE "HAKUNA", UTAFUKUZA WATEJA
Unajisikiaje unapoenda duka fulani zaidi ya mara tatu na kukosa mahitaji yako, ila ukienda maduka mengine unapata?
Katika huduma zetu za kushauri wajasiriamali wenye mitaji wanaotaka kuanzisha biashara za dawa na vipodozi tunakutana na mambo mengi sana, ila kubwa la kwanza ni ishu ya mtaji na kupangilia matumizi yake. Swali kubwa ni kwamba “Natakiwa niwe na mtaji kama kiasi gani unaotosha kuanzia?”.
Sasa ukiwa na mtaji unaotosha kuanzia kifuatacho ni kukodi eneo, kufanya ukarabati, kupata wafanyakazi, kupata leseni na vibali, kuweka dawa na/au vipodozi na kujitangaza ili upate wateja wa kuanzia na kuongeza wateja wako.
Biashara ni rahisi sana, na ni mambo makuu matatu:
Bidhaa/Huduma ambazo zinakidhi mahitaji ya soko/wateja wako
Wateja/soko la uhakika kukidhi mahitaji yako ya kibiashara
Utaratibu wa kuwafikia wateja wako na kuwauzia bidhaa/huduma zako
Mtaji mkubwa utautumia kwenye kuandaa duka na bidhaa za kuuza dukani kwako. Ila hakikisha haumalizi mtaji wote kwani unatakiwa kubaki na mtaji wa akiba kwa ajili ya kukidhi dharura na mahitaji ya wateja ambayo hukuyagundua mwanzo wakati unapanga mipango yako. Kwa mfano umeweka losheni za Nivea, Vaseline, Dove na Rubee. Losheni za Rinju hukuweka aidha kwa kusahau au kwa kudhani hakuna wateja wake. Then boooommmmmm…. wateja wa Rinju kibao. Na kila wakija unawajibu hakuna, wanaondoka.
Unatakiwa uchukue hatua ya haraka sana kukidhi mahitaji ya wateja hawa kwani vinginevyo utawakosa moja kwa moja. Unatakiwa utumie mtaji wa akiba ambao uliutenga spesheli kwa ajili hii. Hutakiwi kutumia mtaji wako wote na kubaki bila hela, unatakiwa kubaki na mtaji kidogo kwa kwa ajili ya akiba kama hizi.
Kwa hiyo kwa mfano kama una mtaji Tsh 30,000,000 unataka kuanzisha famasi basi tumia Tsh 25,000,000 kufanya mambo yako yoooote, kisha Tsh 5,000,000 iache tu kama mtaji wa akiba. Mtaji huo utakusaidia kununua dawa ambazo wateja watazikosa, kulipa wafanyakazi kama mauzo bado hayajawa mazuri na matumizi mengine. Usitumie Tsh 30,000,000 yote na kisha ukabaki bila hela.
Kama una mtaji wa Tsh 4,000,000 na unataka kuanza biashara ya vipodozi basi tumia Tsh 3,000,000 hadi Tsh 3,500,000 kwa mahitaji yako yoooooote, kisha hiyo Tsh 500,000 iache kama mtaji wa akiba. Usitumie Tsh 4,000,000 yote na kisha ukabaki bila hela.
Jipange vizuri. Kuwa tayari kwa mahitaji yatakayojitokeza. Pata ushauri.
#hospitali